Mheshimiwa Dr. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri Mteule Wa Kilimo |
Kamati
ya uongozi inayoshugulikia ujenzi wa jiji la sayansi, teknolojia na ubunifu la
Tanzanite City – Chunya, pamoja na wadau wetu wote kupitia klabu ya marafiki wa
Tanzanite City, tunapenda kutoa pongezi zetu za dhati kabisa kwa mbunge wetu wa
Mbeya na mdau wa Tanzanite City, Mheshimiwa Dr. MARY MWANJELWA kwa kuteuliwa
kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli Kuwa
Naibu Waziri wa Kilimo.
Tunatambua
uwezo mkubwa sana alionao Mh. Mwanjelwa katika kutekeleza majukumu yake. Sisi kama
wadau wa maendeleo ya viwanda na Teknolojia tunatambua jukumu kubwa na zito
analokwenda kulibeba Mh Mwanjelwa, si mchezo-mchezo bali anatakiwa kuwa mbunifu
sana na asiyechoka kujifunza. Nchi yetu ni kubwa sana na ina matatizo mengi mno
yanayohusiana na wizara anayokwenda kuifanyia kazi.
Moja
ya changamoto ambazo Mh. Naibu Waziri atakutana nazo katika utekelezaji wa
majukumu yake ni matumizi duni ya teknolojia katika kilimo kwa ujumla wake na namna
ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Katika wakati huu ambao taifa letu lipo
kwenye kipindi cha mpito kuelekea uchumi wa kiviwanda, suala la teknolojia
linapaswa kupewa kipaumbele kwani linagusa kila Nyanja ya kilimo, kuanzia
kwenye maandalizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuilima, kupanda na kupandikiza
mazao mashambani, kutunza mazao yaliyoshambani ili yaweze kutoa matunda bora na
ya kutosha, uvunaji wa mazao na kuyasafirisha toka mashambani, uhifadhi wa
mazao ghafi ya kilimo pamoja na kuyaongezea thamani. Yote hayo yanahitaji
teknolojia kwa mapana yake!
Mh.
Naibu Waziri, ni vigumu sana kuweza kuendelea kama taifa, iwe ni kwenye kilimo,
viwanda au hata biashara tu, iwapo tutapuuza matumizi ya teknolojia. Lakini pamoja
na kutilia maanani matumizi hayo ya teknolojia, bado hatutaweza kufikia malengo
yetu ya kiuchumi kama tutaendelea kuwa tegemezi kwa kiteknolojia toka nje. Kwani
hao tunaowategemea wao pia wanavyo viapaumbele vyao ambavyo siyo lazima
vifanane na vyetu. Hivyo sasa ni jukumu letu kama kweli tunataka kwenda kwenye
uchumi wa kati, wa viwanda na kilimo cha kibiashara na chenye tija, kuanza sasa
kujenga uwezo wetu wenyewe kwenye mambo ya technolojia ambao ndiyo mhimili wa
hivyo viwanda na hicho kilimo tunachokitaka.
Mh.
Naibu Waziri, sisi tumeanza na Tanzanite City, ni safari ngumu na ndefu, lakini
tumedhamiria kufika mwisho, tunaamini kuwa, kwa kuwekeza kwenye vipaji vya
vijana wetu, na kuwasaidia kutimiza ndoto zao, tutabadilisha mustakabari wa
taifa letu na kuboresha sana kilimo chetu, tukishirikiana sisi wanachi, wadau
wa maendeleo, pamoja na serikali tunaweza kuifanya Tanzania kuwa kiwanda cha
Afrika, na kitovu cha ubunifu katika maswala ya teknolojia.
Mh.
Naibu Waziri, tuna jua NIA UNAYO, SABABU UNAYO NA UWEZO UNAO! Tunakuahidi ushirikiano
wetu, tunakuombea afya njema, hekima, na heshima kwa watu unaowaongoza, wengi
wamepita na hawajaacha alama yoyote baada ya wao kuondoka, na wewe hutaishi
milele kwenye hiyo nafasi, lakini tunatamani kuona alama za kazi zako zikidumu
daima kwa vizazi vingi vijavyo!! TUNAJUA NA TUNAAMINI UNAWEZA!!! Tuna kutakia
kila lililo la heri, ufanikiwa katika majukumu yako hayo kwa taifa letu, MUNGU
Akubariki na akulinde siku zote za maisha yako. Amina.