Bundi: Alama/Ishara ya ushirina na uchawi |
Mapinduzi ya kiteknolojia yanatokana na kazi za utafiti wa kiasayansi na siyo matunguli |
Wakati wanasayansi wenzetu wanaota kuishi nje ya sayari ya dunia, sisi tunamikakati gani ya kuelekea huko? |
Wakati
ambapo baadhi ya watu waliofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika maisha wakionekana
kama mfano wa kuigwa katika jamii yetu kuna jamba moja ambalo kwa kweli linatia
hofu japo kwa sasa inaonekana kama sehemu muhimu sana katika maisha. Sio ajabu
hapa nchini kusikia kuwa baadhi ya watu maarufu wakiwemo wanasiasa,
wafanyabiashara na wafanyakazi bila kujali kiwango cha ufahamu au elimu zao
kuwa mafanikio waliyonayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu za giza!
Tumeshazowea kushuhudia wanasiasa wakipishana bila idadi kwa sangoma kule
mlingotini wakisaka ubunge au madaraka mengine ya kisiasa! Inashangaza sana
kwamba viongozi wetu hawaamini kama watu waliowachagua walifanya hivyo hivyo kwa
kuwaamini matokeo yake wanatafuta mbinu za kichawi ili kuwaroga wapigakura wao
au mabosi wa ili wawachague na kuwapa ulaji wanaoutaka. Tunajua viongozi wengi
ambao wanapata madaraka kwa njia za kichawi, mara nyingi hawajiamini kwenye
manbo ya kimsingi lakini majibu yao yamejaa kiburi, jeuri na kejeli, wanajua
watu waliowapa madaraka walionayo hawana uwezo wa kuwaondoa kwani hata hivyo
hawakuwapa kwa dhamira zao binafsi bali kwa nguvu za giza
Wafanyabiashara
kwa upande wao nao kila kukicha wanashindana kwa waganga kutafuta madawa ya
kuvuta utajiri zaidi na kung’arisha nyota zao, wao wapo tayari hata kutoa uhai
wa binadamu wenzao ilimradi tu wapete mali zaidi, huu ni ubinafsi uliovuka
mipaka kiasi ambacho huwezi kuelezea, wengine wamedirika hata kufanya ngono na
wazazi wao ili wapate hiyo mali na utajiri wanaousaka usiku na mchana. Hali
haiko tofauti huko maofisini, ambako wafanyakazia katika kada mbalimbali nao
wanakesha kwa wataalam kutafuta bahati ya kupandinshwa cheo, kulinda kazi zao
zisiwaponyoke, au kuongezwa mishahara na kupewa upendeleo katika mambo
mbalimbali ya kikazi. Kwa maaskofu na mashehe huko hali ndiyo mbaya zaidi, sasa
siyo ushirikina peke yake, wapo baadhi wanauza hata madawa ya kulevya kupitia
makanisa yao!
Hali
inatisha zaidi pale serikali inaposhadadia nguvu zisizoonekana kwa kisingizio
cha kuiombea nchi, wanasiasa hawajiulizi mara mbili kuwakusanya wananchi kwa
maelfu kufanya maombi pale taifa linapokabiliwa na tishio fulani iwe la
kisiasa, kiuchumi au kijamii. Kwenye michezo hili ndiyo imekuwa ada, bila
maombi timu zetu hakuna kitu, utamsikia kiongozi wa soka akiwahimiza wananchi
“ndugu wananchi tuiombee timu yetu ya taifa katika mchezo wa leo iweze kushinda
kwani mchezo huu ni wa muhimu sana…” utadhani wapinzani wetu wao hawamjui Mungu
au tunategemea mwenyezi Mungu amtume roho mtakatifu kama alivyofanya kwa wale
mitume 11 wa bwana Yesu ili waweze kucheza na kupata ushindi. Naomba hapa
ieleweke kwamba sipingi kumuomba mwenyezi Mungu kwa lolote lile, tatizo langu
liko kwetu sisi wenyewe, kuwa tumefanya nini kilichondani ya uwezo wetu kuweza
kufanya vizuri kabla hatujamgeukia Mwenyezi Mungu? Au ndiyo tunategemea muujiza
kama ule wa babu wa Loliondo? Hii
inatisha sana hasa kwa taifa changa kama letu ambalo tunahitaji kukimbia
kisayansi na kiteknoljia wakati wenzetu wanatembea ili tuweza kuondoa pengo la
kimaendeleo baina yetu na mataifa mengine.
Mganga wa kienyeji mitaani Afrika Kusini |
Pengine hatuwezi kushangaa sana kuwa
hata serikali inashabikia imani za giza, kwa kuwa baadhi ya hao viongozi
wanaoongoza hiyo serikali yenyewe pia wanaamini kuwa madaraka yao yametokana na
msaada wa kichawi au nguvu za giza. Tunategemea nini kipya toka kwa viongozi
kama hao? Tutakuwa wehu kama tutafikiri kuwa watu wanaweza kubadilika na
kusaliti miungu wao, kamwe hawawezi kukemea mambo hayo pamoja na ukweli kuwa
wanaelewa vema madhara yake kwa taifa letu na vizazi vyake.
Lakini labda mtu anaweza kujiuliza
kuwa “ni kwa nini tunapinga imani hizi za kishirikina wakati kuna watu wengi
wameweza kupata mafanikio makubwa sana na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo
ya taifa?”
Kwanza kabisa ni lazima tuelewe kuwa
ushirikina ni ishara ya wazi ya mtu aliyeshiwa mbinu na mikakati ya kimaisha,
ni alama ya mtu ambaye hana jipya katika fikra zake na amefika mahali haoni
suluhu yoyote ya matatizo yanayomkabili iwe ya kiuchumi, kijamii, kisiasa au
hata mahitaji ya binfsi ya kibinadamu. Mtu anapofikia hatua hiyo hukabliwa na
msongo wa mawazo na ni rahisi sana kushawishika kuingia kufanya jambo lolote
lile litakaloelekea kumpatia ahue ya muda bila kujali athari za baadaye za
matendo yake.
Wataalamu wakifanyia majaribio "Memory" ya simu ya mkononi, ushirikina hauwezi kwenda sambamba na kazi za kisayansi! |
Jambo moja kubwa ambalo tunaweza
kujifunza kutokana na biashara hii ya nguvu za giza na ambalo linaweza kuwa na
manufaa makubwa jamii yetu ni namna watu hawa wanavyoweza kucheza na akili wa
watu na kufanya kila kitu kionekane kuwa halisia, hisia hizo huwafanya watu hao
kuwa na imani kubwa kiasi ambacho hawaamini kabisa kwamba kuna kushindwa katika
maisha wakiwa na nguvu za giza. Nguvu hizo huwa kubwa kiasi cha kumfanya
muhusika kufanya jambo lolote katika maisha bila kujali kupata athari mbaya,
watu hawa huvaa ushujaa ambao unawafanya wasiweze kushindwa kitu. Lakini
kutokana na ukweli kuwa watu wetu hawana elimu ya jinsi akili na ubongo wa
binadamu unavyofanya kazi wanadhani ni damu za mbuzi au viungo vya albino
vinavyowaletea mafanikio, jambo ambalo yawezekana likawa na ukweli japo ni
kweli pia kuwa waganga wengi ni matapeli na dawa zao hazina owezo huo.
Uchawi pia unahusishwa na nguvu na uwezo wa ajabu unaopita uhalisia wa kibinadamu |
Watu ambao tumekuwa tukidhani kuwa ni
wasomi na wataalamu wa mambo mbali mbali katika jamii na ambao tunawamini
kutushauri kila siku kwenye biashara zetu n.k. utkakuta kuwa wao wenyewe hawana
kitu na hata hizo biashara wanazoshauri wao hawazifanyi – utakutana na mtaalamu
elekezi wa biashara anashauri juu uendeshaji wa maduka lakini yeye menyewe hata
genge linamshinda kusimamia. Tunayaona haya kwenye mikataba mbalimbali ambayo
wataalam wetu wanaiingizwa mkenge aidha kwa makusudi au kwa kutojua. Wanahubiri yale wasioyatenda, ambavyo wao
wenyewe hawayaamini lakini mwisho wa siku lawama zote wanatupiwa wananchi
masikini kwa ujinga wao.
Safari ni ndefu lakini lazima tuianze
sasa! Hatuna muda zaidi wa kusubiri vinginevyo tuwe tayari kujisalimisha kwa
wakoloni kwa mara nyingine watutawale na kutupa mkate wa siku huku tukiwa
makolokoloni na mayaya majumbani kwao na wao akifanyakazi kwenye miradi ya
kuhamisha rasilimali za taifa letu.
No comments:
Post a Comment