Search This Blog

TANZANITE CITY: The Africa's Factory & Innovation Powerhouse!

TANZANITE CITY: The Africa's Factory & Innovation Powerhouse!
We Will Turn Bushes Into Highly Industrialized City

Monday, November 18, 2013

Maendeleo ya teknolojia hayaji kama mvua, tujitoe tuwekeze!



Wakati taifa letu lina umri wa zaidi ya miaka 50 tangu tujitwalie uhuru toka kwa wakoloni mwaka 1961, nadhani ni wakati mwafaka kwetu watanzania kujiuliza  kama kwa muda wote huo ni nini tumefanya kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu, je hapa tulipo ndipo tulipotarajia kuwepo? Kama jibu ni ndiyo je sasa tunaelekea wapi na tutafikaje! na kama jibu ni siyo, ni kwanini tupo hapa na tunafanya nini ili kurudi kwenye mstali wa matarajio yetu? Ili tuweze kuelewa vizuri mantiki ya kujiuliza haya ni vema tukaweka mbali ushabiki wa kisiasa na siasa zisizokuwa na tija kwa kuzungumzia watu badala ya mambo ya msingi yanayoligusa taifa letu. Nasema hili kwani ni kawaida yetu kuingiza siasa kila mahali hata ambapo haistahili kuwepo siasa, watu waliofilisika kifikra wakati wote wao wanafikiria kulinda au kujenga “status” zao tu na kwa gharama yoyote ile bila kujali maslahi mapana ya taifa letu, watu hawa ni hatari na hawafai kuendekezwa kwani kwao kila jambo ni siasa tu.

Uundaji wa wa ndege kubwa kuliko zote duniani kwa sasa Airbus 380 ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa kwa pamoja na kwa ushirikiano baina ya wanasayansi, serikali na wadau wengine
 Katika nchi yetu hivi sasa kumefurika bidhaa za kila aina kutoka kila kona ya dunia, miongoni mwa bidhaa hizo ni zina toka katika mataifa ya mashariki ya mbali yakiongozwa na ndugu zetu wachina, hivi sasa Tanzania tunaagiza toka nje karibu kila kitu kuanzia vijiti vya kuchokolea meno, pamba za kusafishia masikio hadi zana za kisasa za teknolojia ya hali ya juu kama eropleni za mizigo na abiria magari meli kompyuta, simu vifaa vya kitabibu nk. Nyingi ya bidhaa hizo hazina ubora maridhawa maarufu kama bidhaa za kichina, kwani hazidumu kwa muda mrefu kama ilivyozoeleka kwa bidhaa tooka nchi za kimagharibi yaani ulaya na marekani. Kwa jumla ni kwamba wachina kwa sasa ndiyo wanaotawala soko la bidhaa za kiteknolojia hapa nchini na ni ukweli usiopingika kwamba hivi sasa wachina wanagusa maisha ya kila raia wa Tanzania kwa bidhaa zao, na naweza kwenda mbali zaidi kuwa hata watoto ambao hawajazaliwa, tumboni mwa mama zao, maisha yao yanaguswa na uwepo wa bidhaa za wachina.
Hali hii ya wachina kutawala soko la teknolojia hapa nchini siyo bahati mbaya wala haikuja kama mvua tu, bali ilikusudiwa na kuwekewa mikakati ya makusudi kabisa na selikali ya uchina na kufanyiwa kazi kwa dhati kabisa. Moja ya mikakati mkubwa ya serikali ya uchina ilikuwa ni kuvutia uwekezaji wenye tija katika maeneo maalum ambayo waliyachagua na kuyapa kipaumbe, wakati huo huo walihakikisha kuwa wataalamu wao hasa wahandisi wabunifu wanapatiwa fursa za kuwawezesha kujifunza toka kwa wawekezaji wakigeni kwa kufanya nao tafiti mbalimbali pamoja na kuendesha miradi kwa ubia kati wageni na wenyeji. Serikali ya china ilihakiksha inawapatia rasilimali za kutosha wataalam wake kuweza kunyumbulisha teknolojia walizojifunza kwa manufaa ya taifa lao. Serikali ya china pia ilihakisha kuwa sera na sheria za nchi zinasaidia zaidi kuwalinda wanasayansi wao na kuwapa msaada wa kila namna ili waweze kushindana kibiashara. Matokeo yake kila mtu anayajua, dunia nzima hivi sasa zimeenea bidhaa za kichina, Leo hii chochote utakacho fikilia katika masuala ya teknolojia utakipata uchina. Sisi je? Tupo wapi?

Wanafunzi mafunzoni: Wanaunda boti kama sehemu ya mafunzo.

Bila shaka tutakubaliana kwamba walichokifanya wachina sio uchawi, bali ni matokeo ya nia, madhumuni, jitihada na maamuzi magumu na makini waliyoyafanya. Nasema maendeleo na mafanikio ya uchina ya leo ni matokeo ya nia, madhumuni, jitihada na maamuzi magumu na makini yaliofanywa na viongozi wao miaka ya hamsini na sitini lakini yaliyotiwa nguvu mpya mwaka 1978 kwa mikakati ambayo imezaa mafanikio haya tunayoshudia leo.
Watanzania tunaweza kuwa kama au hata zaidi ya wachina kimaendeleo tukiamua, tunaweza kujifunza toka kwao kama tukitaka, tunaweza kufanya maamuzi magumu na makini sasa kwa manufaa ya vizazi vijavyo tukipenda. Nasema tukitaka au tukipenda kwa kuwa hatulazimishwi kufanya hayo, yote ni hiari yetu, hakuna atakaye tuuliza kwa nini hatuja fanya wala atakayetulaumu kwa kufanya. Lakini tukiamua kufanya basi tuweke siasa pembeni na tufanye kazi, kwani hatima yetu na  ya taifa letu imo mikononi mwetu. Tunaweza kuibali kama tutaamua kufanya hivyo, vinginevyo tunaweza kuendelea kupiga siasa kwenye kila kitu tunachofanya na kucheza michezo michafu na kujipendekeza kwa kina Fulani tukidhani watatuona wa maana na tunajua sana,  tusipo fanya tutaendelea kulaumu sana wakoloni na wachina, tutaendelea kuabudu mlingotini na kugombana kwa dini na makabila yetu wakati mifano tunayo dhahili.
NDUGU ZANGU TUAMUE SASA KUBADILIKA, TUTAKE TUWE KAMA WACHINA, TUNAJUA TUNAWEZA, SABABU TUNAYO, NIA TUNAYO NA RASILIMALI ZOTE TUNAZO, TUSIPOZITUMIA SISI RASILIMALI ZETU WATAZITUMIA WENGINE NA HATUTAWAZUIA! TUTABAKI TUNALALAMA TU HADI LINI?

No comments:

Post a Comment