Tunapozungumzia teknolojia tuangalie katika namna kubwa mbili; Teknolojia ya viwanda vinavyozalisha bidhaa za mwisho kwa ajili ya walaji, Teknolojia ya viwanda mama vinavyozalisha mitambo na mashne za uzalishaji
Taifa letu hivi sasa lina umri wa miaka 50 tangu tupate uhuru toka kwa mkoloni, mpaka sasa hakuna uwekezaji wowote wa uhakika uliofanywa katika kukuza teknolojia ya viwanda nchini zaidi ya ule uliofanyika wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi wa taifa letu iliiyoongozwa na hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Uwekezaji katika namna ya Kwanza ya teknolojia ni rahisi kidogo kwani hutegemea zaidi na hali na mazingira ya soko, aina ya bidhaa na uwezo wa mtaji wa mwekezaji. Uwekezaji huu unaweza kufanywa na mtu yoyote, ni wa kibiashara zaidi na unalenga kuzalisha bidhaa mahususi. Taifa linapojikita zaidi katika uwekezaji wa namna hii litakabiliwa na matatizo yafuatayo; Mitambo na mashine za viwanda hivi hununuliwa kama zilivyo toka nchi zinakotengenezwa, taifa linalonunua linategemezi kiteknolojia kwa vile muuzaji wa mitambo hiyo ndiyo mwenye teknolojia na ndiyo wanaofanya tafiti na kuendeleza teknolojia hiizo, Taifa linapowekeza katika viwanda vya namna ya kwanza linatumia gharama kubwa sana kuboresha teknolojia ya mitambo na mashine zake na mara nyingi hufanya hivyo baada ya kupitwa na wakati kwa mbali sana, hivyo viwanda hivyo huendeshwa na soko badala ya kuliendesha soko, Taifa linapowekeza zaidi katika viwanda hivi bila kuwekeza katika utafiti wa teknolojia na viwanda mama ambavyo ndiyo huviwezesha viwanda hivyo kiteknolojia, basi viwanda hivyo haviwezi kuhimili ushindani katika soko huria ambalo limejaa bidhaa toka kila kona ya dunia
Lakini uwekezji katika namna ya Pili, yaani teknolojia mama, ni mgumu na wa gharama kubwa sana kwani unagusa fani nyingi tofauti tofauti na wakati mwingine ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na bidhaa lengwa. Kwa jumla tunapozungumzia kuwekeza kwenye technolojia ya viwanda mama tunapaswa kufikiria mfumo mzima wa utafiti na uendelezaji teknolojia. Mfuno huu unahusisha miongoni mwa mambo mengi, yafuatayo; Ukusanyaji wa taarifa za kisayansi na teknolojia (Intellectual Property Resources and Technology Transfer), utunzaji wa taarifa hizo na namna ya kuzifikisha kwa walengwa ambao ndiyo watumiaji, Tafiti za kisayansi (Research & Development) na namna unavyowawezesha wataalam kufanya tafiti, kujaribu mawazo yao na kuunda vifaa vipya kwa ajili ya majaribio ya kisayansi, Ubunifu na usanifu (Design, Development and Innovation) wa bidhaa na mifumo mipya ya ualishaji na namna ya kuhakisha ubora na viwango
Tunapozungumzia uwekezaji katika teknolojia hatumaanishi wawekezaji wageni ambao wao dhamila yao kubwa ni kukusanya faida kubwa iwezekanavyo toka kwenye kile wanachowekeza na siyo kuinufaisha nchi, tumeona jinsi wawekezaji wanavyofanya kila linalowezekana kukwepa kulipa kodi za serikali pamoja na faida kubwa wanayoipata kutokana na rasilimali zetu. Uwekezaji unaofanywa na watu hawa ni ule tu unaowaongezea wao tija, nafasi ya kuaminika na kujiongezea faida zaidi.
Tunaposema tuwekeze katika teknolojia tunamaanisha; kusomesha wataalam wetu wenyewe, kuthamini kazi za wataalam ambao tayari tunao na kuwahakikishia mazingira mazuri ya kazi, kuwapatia wajasiliamali wetu mitaji bila kujali itarudi lini na kuwawezesha kiteknolojia. Swala hili ni gumu sawa kabisa na swala la kusomesha watoto kwa mzazi asiyejua maana ya elimu kwa wanawe. Mzazi huyu anaona mzigo kutoa sehemu ya mapato yake kusomesha watoto wake mwenyewe kwa kuwa tu, hata waliosoma au kusomesha wa kwao nao pia bado wanamaisha magumu. Lakini mzazi huyo huyo ndiyo wa kwanza kusifia mafanikio ya watoto wa jirani zake.
Watanzania ni lazima tuamue sasa kuwekeza kwenye teknolojia ama sivyo tuache kuota ndoto za maendeleo, vinginevyotutakuwa tunasubiri matokeo ya bahati nasibu yatangazwe kwa matumaini ya kushinda wakati hatukukata tikiti.
Moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wajasiliamali wa Tanzania ni ubora duni na gharama kubwa sana za uzalishaj,i bidhaa za wajasiliamali wetu haziwezi kuhimili ushindaji hata katika soko la ndani tu. Katika hili kuna mambo makubwa mawili; Ubora na Gharama.
Tatizo la ubora linasababishwa zaidi na ufinyu wa mitaji na teknolojia hafifu zinazotumiwa na wajasiliamali wengi wa Tanzania, kukosekana kwa taarifa za kiteknolojia (Intellectual Property Resources), kukosekana kabisa kwa mifumo ya kufuatilia ubora na viwango vya malighafi na vifaa vya uzalishaji.
Vilevile uhaba wa wataalamu mbalimbali katika teknolojia kunapelekea ubora duni na gharama kubwa za uzalishaji katika viwanda vyetu vingi. Tanzania hatuna mfumo mzuri wa kuwatumia vizuri wataalamu wetu hasa wastaafu ambao ujuzi na uzoefu wao ungeweza kuwa nguzo muhimu sana katika ujenzi wa taifa letu. Hivi leo siyo ajabu kukutana na mtu uliyesoma naye darasa moja chuo kikuu wakati huo mkichukua degree ya uhandisi mitambo, akakuambia yeye ni mwanasheria au mhasibu wa taasisi fulani na hataki hata kusikia habari ya uhandisi. Haya yote ni matokeo ya kukosekana kwa uwekezaji wa uhakika kwenye teknolojia ya viwanda mama
Baada ya wajasiliamali kufanikiwa kutengeneza bidhaa zao, tatizo lingine ni namna ya kuziingiza sokoni, Tanzania hatuna mfumo madhubuti wa kuwaingiza sokoni wajasiliamali wazalendo zaidi ya maonyesho machache ya kibiashara yanayofanyika katika baadhi tu ya sehemu hapa nchini. Tumekuwa tukisikia mara nyingi viongozi wakisema “zalisheni bidhaa kulingana na mahitaji ya soko” bila ya kuainisha hayo mahitaji ya soko, lakini wakati huo huo wachina wanauza kila kitu katika soko hilohilo ambalo sisi tunashindwa kuuza, Mimi naamini kuwa katika teknolojia fursa huwa haziishi na kila kitu cha kiteknolojia kinaweza kuuzika bila kujali kimetoka wapi, cha msingi ni ubora na gharama, kisha kinachofuata ni mfumo wa kuuza ambao kwa bahati mbaya hatunao.
Kimsingi watanzania wote sasa tunawajibika kuchukua hatua kila mmoja kwa nafasi yake kwa kushirikisha serikali, na wadau wengine wa maendeleo kuweka mazingira mazuri kwa wataalam wetu na kuwaleta pamoja wanasayansi, wahandisi, wahitimu a vyuo vikuu, wajasiliamali na wadau wengine katika kutafuta majibu ya kiteknolojia kwa matatizo na changamoto zilizopo katika jamii zetu. Serikali kwa upande wake inapaswa kuweka vipaumbele kwa wawekezaji wanje kwenye maeneo yale tu ambayo yatatusaidia kuwapatia wataalam wetu ujuzi na utaalam hasa kwenye eneo la teknolojia ya hali juu sana (hi-tech). Ikibidi kuwe na utaratibu maalum wa kuwaelekeza wawekezaji maeneo mahsusi ambayo wataalam wetu watajifunza na kuambukizwa teknolojia ambayo nao wataitumia kwa manufaa ya taifa. Kwenye hili tutapata tabu sana hasa kwenye masuala ya haki miliki, lakini lazima tujue kwamba kwa sasa kila mtu anatamani kuwa rafiki yetu iwe wa kinafiki au wa kweli, hivyo huu ndiyo wakati wetu tunaopaswa kuchuma kutokana na lasilimali zetu vinginevyo tutaliwa! Asietaka kufungua haki miliki zake ili afaidike na rasilimali zetu tumwache aende wako wengi tu wengine watakuja, wala hatuna haja ya kufanya haraka, kwani rasilimali zetu aziozi wajukuu zetu watazikuta kama sisi tulivyozikuta. Ninaposema tuwekeze kwenye teknolojia sina maan kwamba tukianza kuwekeza leo, basi kesho tutaweza kuunda jeti, hapana. Maana yake ni kuwa tukianza kuwekeza sasa na kuweka mazingira bora kwa wataalam wetu kupata teknolojia hizo itakuwa ni mtaji mzuri sana hapo baadaye kuweza kuunda vifaa vya teknolojia ya hali ya juu sana kama vile ndege za jets.
Serikali inahitaji kueweka utaratibu mahsusi wa kusimamia tafiti za kisayansi, kugharamia uendelezaji wa teknolojia na kusomesha wataalamu kulingana na mahitaji ya wakati husika, Kuondoa pengo la kiteknolojia kati ya nchi yetu na mataifa yaliyoendelea, kwa kufanya uchunguzi wa kiintelijensia kujua ubunifu na hatua zinazofanywa na wanasayansi kwingineko duniani ili kuepuka mshangao (surprise) toka kwa washindani wetu. Kushiriki kikamilifu katika kufanya tafiti na kuendeleza teknolojia muhimu kwa mahitaji ya wananchi wa mijini na vijijini, kukuza uwezo wa wajasiliamali kuanzisha na kuendesha biashara za uzalishaji kiushindani na kwa ufanisi, kuhamasisha kuanzishwa kwa viwanda vingi vidogo vidogo ambavyo vitatumia teknolojia rahisi kuvuna rasilimali zetu kwa manufaa ya wote na sio watu wachache wenye uwezo, pia kulinda na kutunza mazingira yetu
Tunahitaji kuwa na taasisi za kutosha ambazo zitakuwa kama macho yetu kwa ulimwengu wa nje wa sayansi na teknolojia, kwa lengo la kukusanya, kutunza na kusambaza taarifa za kisayansi na kiteknolojia kwa wadau pale zinapohitajika kwa wakati na ubora.
Tunahitaji vituo mbalimbali vya kusimamia na kuendesha tafiti mbali mbali za kisayansi (mbali ya vyuo vikuu), kufanya majaribio ya kisayansi na kubuni na kuzifanyia utafiti teknolojia mbali mbali na kuzitolea taarifa (Technical Reports)
Vituo vya Usanifu na Ubunifu - Design, Development & Innovation Administration; vituo hivi vinajukumu kuwasaidia wataalamu na wajasiliamali wetu la kutafsiri matokeo ya tafiti za sayansi na teknolojia kuwa katika vitu halisi, inawajibika kubuni bidhaa mbali mbali kutokana na matokeo ya tafiti na mahitaji soko, kuandaa michoro pamoja na kutengeneza prototype, na kufanya majaribio na mpangilio wa uzalishaji. Kubuni na ketengenza mfumo mzima wa uzanishaji wa vifaa husika ili kukidhi mahitaji.
Vituo vya uwekezaji na msaada wa kiufundi wa viwanda vidogovidogo SMEs Development & Support – kuwasaidia wajasiliamali wa Tanzania kuweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozitengeneza zinakidhi viwango vya ubora na vinaweza kuhimili ushindani wa soko huria